Mgomo wa wauguzi waendelea Siaya

Marion Bosire
1 Min Read

Mgomo unaoendelea wa wauguzi umeingia siku yake ya nne leo katika Kaunti ya Siaya ambapo jana wahudumu wa afya walimiminika mitaani wakiishutumu serikali ya kaunti kwa kupuuza matatizo yao.

Mgomo huo ambao ulisababisha wauguzi kuandamana barabarani na baadaye kupiga kambi kwa muda katika makao makuu ya kaunti, uliathiri kwa muda mfupi harakati za magari, huku waandamanaji wakiahidi kutorejea kazini hadi malalamiko yao yote yatakaposikilizwa na kutatuliwa.

Wakizungumza na wanahabari, maafisa wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi na Wakunga tawi la Siaya, wakiongozwa na mwenyekiti Dennis Omollo na Katibu Mkuu Kennedy Hamisi, waliishutumu serikali ya kaunti kwa kushindwa kutekeleza makubaliano yao.

Makubaliano hayo yalitiwa saini mwezi mmoja uliopita na yakawafanya wakarejea kazini kwa msingi wa kutoa muda wa mazungumzo.

Miongoni mwa masuala wanayotaka yashughulikiwe ni kucheleweshwa kwa mishahara na kutowasilishwa kwa makato ya wahusika wa tatu kwa taasisi mbalimbali.

Katika majibu ya haraka, Gavana wa Siaya, James Orengo alihusisha kucheleweshwa huko na urasimu kutoka Hazina ya Kitaifa, na kuongeza kuwa serikali yake tayari imepokea mgao kutoka kwa hazina hiyo na mishahara yao italipwa haraka iwezekanavyo.

Share This Article