Serikali leo imezindua mpango wa ufadhili unaolenga watu ambao hawajiwezi katika jamii kuwawezesha kupata huduma za afya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo katika ikulu ya Nairobi, Rais William Ruto alisema kwamba mpango huo unahusisha wakenya milioni 2.2 ambao hawawezi kulipa ada ya shilingi 300 kila mmoja.
Wakenya hao sasa watasajiliwa kwenye mamlaka ya afya ya jamii SHA.
Kiongozi wa nchi alisisitiza kwamba serikali yake imejitolea kuhakikisha kwamba huduma za afya zinapatikana hata kwa waliotelekezwa katika jamii.
Rais alisema mpango huo unanuiwa kulinda walio katika hatari katika jamii kutokana na uwezekano wa kusahaulika au kuachwa nje ya mpango mpya wa huduma za afya.
Ruto wakati huo huo alipongeza hatua zilizopigwa na SHA kupitia kwa kuweka usimamizi wa mipango yake yote kwenye mfumo dijitali hatua ambayo inaimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika huduma za afya.
Huku haya yakijiri, Naibu Rais Kithure Kindiki amefanya mkutano na wahudumu wa afya ya jamii wapatao 6500 na wadau wengine wa sekta ya afya katika kaunti ya Meru.
Mkutano huo ulifanyika katika eneo la Irunduni, kaunti ya Tharaka Nithi.