Mshukiwa wa wizi wa kimabavu anaswa Samburu

Marion Bosire
1 Min Read

Maafisa wa upelelezi wa jinai huko Samburu wamekamata jamaa kwa jina Christopher Ayok Lemarkele wa umri wa miaka 20, anayeshukiwa kutekeleza visa kadhaa vya wizi wa kimabavu mjini Maralal na maeneo ya karibu.

Lemarkele ambaye alikuwa amejihami kwa bunduki aina ya AK-47 akiwa na mwenzake aliyekwepa kukamatwa, walivamia duka moja huko Maralal.

Walijisingizia kuwa wateja wa kawaida kabla ya kubadilisha mambo haraka walipotoa bunduki na kumwelekezea mhudumu wa duka hilo ambaye aliweza kusukuma bunduki hiyo huku Lemarkele akifyatua risasi.

Risasi hiyo ilimkwaruza mhudumu huyo kwenye titi lake la kushoto na kumwachia jeraha. Alikimbizwa kwenye hospitali ya rufaa ya Samburu ambako alitibiwa na kuruhusiwa kuondoka akiwa imara.

Polisi walianzisha msako kufuatia kisa hicho ambapo washukiwa waliiba shilingi elfu 50, na wakampata Lemarkele kwenye maficho yake na kumkamata.

Wapelelezi walipata ushahidi mbali mbali kutoka eneo alilokuwa mshukiwa huyo kama vile sare za polisi na vifaa vingine.

Vitu alivyopatikana navyo Lemarkele

Lemarkele atasalia korokoroni huku uchunguzi ukitekelezwa na akiandaliwa kufikishwa mahakamani. Maafisa wa usalama wa Samburu sasa wanamsaka mshirika wake ili naye achukuliwe hatua kisheria.

Share This Article