Rais Ruto asema serikali imeimarisha uchumi

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amesema kwamba utawala wake umefanikiwa kuimarisha uchumi wa taifa hili.

Akizungumza jana Alhamisi jijini Nairobi katika kongamano la kusherehekea miaka 50 ya muungano wa Kiinjilisti wa Kenya EAK, kiongozi wa nchi alisema hata ingawa kumekuwa na changamoto serikali imepiga hatua kubwa.

Alitaja uchumi, usalama, kilimo, huduma za afya, elimu na uunganishaji umeme kama baadhi ya mafanikio yaliyoafikiwa chini ya uongozi wake.

Ruto wakati huo huo alisisitiza kwamba nchi iko katika mkondo ulio sawa na imeweza kuwajibikia majukumu yake ya kifedha ya nje bila kuchelewa.

Rais Ruto alisema pia kwamba serikali yake imefanikiwa kuimarisha sekta ya elimu ya juu nchini kwa kuhakikisha vyuo vikuu vya umma vinashikilia mkondo wa kuhakikisha vinaafikia utoshelevu wa kifedha katika muda wa miaka mitatu ijayo.

Kulingana naye, hilo litafanikishwa na mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya vyuo vikuu. Alisema mfumo huo ambao unaangazia mwanafunzi unatatua changamoto za kifedha ambazo zilikaribia kukwamisha kabisa taasisi hizo za elimu ya juu.

Muungano huo wa makanisa ya Kiinjilisti nchini ulibuniwa mwaka 1975, wakati huo ukijulikana kama Ushirika wa Kiinjili wa Kenya yaani Evangelical Fellowship of Kenya na baadaye ukabadilishwa jina kuwa Muungano wa Kiinjilisti wa Kenya yaani Evangelical Alliance of Kenya mwaka wa 2002.

EAK ina usajili wa zaidi ya madhehebu 900, mengi kati yao yakiwa na uwakilishi wa kitaifa na yaliyosambaa kote nchini. Idadi ya jumla ya waumini wa Kiinjilisti nchini Kenya inakadiriwa kufikia milioni 10.

Share This Article