Umoja wa Milki za Kiarabu, UAE, umeiweka Uganda kwenye orodha ya marufuku ya viza kwa mwaka 2026, na hivyo kuzuia raia wa Uganda kuomba viza za utalii na kazi kuelekea nchi hiyo ya Ghuba.
Hatua hii ni sehemu ya marufuku pana inayokumba nchi tisa ambazo ni Afghanistan, Libya, Yemen, Somalia, Lebanon, Bangladesh, Cameroon na Sudan, kulingana na waraka wa hivi karibuni kutoka idara ya uhamiaji ya UAE.
Marufuku hii haihusu raia wa Uganda ambao tayari wanaishi UAE wakiwa na viza halali, huku mamlaka za UAE zikieleza kuwa marufuku hii ni ya muda tu, ingawa hawajatoa tarehe maalum ya kuiondoa.
Marufuku hii ya viza inajiri baada ya uchunguzi wa kushtua uliofanywa na BBC, uliobaini biashara haramu ya usafirishaji na unyanyasaji wa wanawake wa Uganda walioko Dubai.
Uchunguzi huo ulibaini kuwa operesheni hizo zilikuwa zinaendeshwa na mtu aitwaye Charles Mwesigwa, aliyekuwa akiwahadaa wanawake kwa ahadi za kazi halali, lakini anawalazimisha kuingia kwenye biashara ya ngono wakiwa na madeni makubwa na wakiteswa na wateja matajiri.
Ushuhuda wa kusikitisha ulihusisha simulizi za wanawake waliodaiwa kudondoka kutoka majengo marefu na kufariki katika hali za kutatanisha, kama vile Monic Karungi na Kayla Birungi.
Wanawake hao wawili, walikwenda Dubai kwa matumaini ya kupata maisha bora lakini wakafa katika hali ya kusikitisha, na familia zao zinadai kuwa vifo vyao havikuchunguzwa ipasavyo.