Mahakama moja mjini Malindi, kaunti ya Kilifi imewaruhusu maafisa wa upelelezi kuendelea kuwazuilia washukiwa wanne wa dhehebu la Binzaro kwa siku 60 zaidi ili kuwawezesha maafisa hao kukamilisha uchunguzi wao.
Hakimu Mkuu Joy Shiundu Wesonga pia amewaagiza maafisa wa polisi kuwazuilia Kahndi Gharama, Thomas Mukonwe, James Kahndi Kazungu na Sharleen Tembo Anindo katika vituo tofauti vya polisi katika kaunti ya Kilifi.
“Ombi la Septemba 2, 2025 limekubaliwa. Washtakiwa nambari 8, 9, 10 na 11 wataendelea kuzuiliwa kwa siku 60 zaidi ili kuruhusu maafisa wa upelelezi kukamilisha uchunguzi, na washukiwa watazuiliwa katika vituo vya polisi vya Ngerenya, Kilifi, Watamu na Kijipwa mtawalia au kituo chochote cha polisi kilichopo katika kaunti ya Kilifi kama itakavyoamuliwa na wapelelezi,” aliagiza Wesonga.
Kesi hiyo itatajwa Oktoba 2, 2025.
Vifo kadhaa vimeripotiwa kutokea katika eneo palipo dhehebu la Binzaro na uchunguzi wa kubaini jinsi vilivyotokea unaendelea kwa sasa.