Mabingwa wa Dunia katika mita 10,000 Beatrice Chebet na Faith Kipyegon wa mita 1,500, watakutana leo kwenye nusu fainali ya mita 5,000, huku mashindano ya Riadha Duniani yakiingia siku ya sita mjini Tokyo, Japan.
Chebet ambaye pia ni bingwa wa Olimpiki katika mbio hizo za mizunguko 12 unusu atashiriki mchujo wa kwanza kuanzia saa saba adhuhuri pamoja na Margaret Akidor anayeshiriki mashindano ya Dunia kwa mara ya kwanza.
Kipyegon ambaye alishinda taji ya nne ya Dunia katika mita 1,500 atashiriki mchujo wa pili pamoja na mshikilizi wa rekodi ya Dunia ya kilomita 10 Agnes Jebet Ngétich aliyemaliza wa nne katika fainali ya mita 10,000.
Kenya ni ya pili kwenye msimamo wa medali kwa dhahabu 4, fedha 1 na shaba 2, nyuma ya Marekani yenye dhahabu 7, fedha 1 na shaba 2.
Makala ya 20 ya mashindano ya Riadha Duniani yatakamilika Jumapili hii Septemba 21.