Katibu katika Wizara ya Masuala ya Vijana Fikirini Jacobs amefichua kuwa serikali imo mbioni kulinda uvumbuzi wa vijana ili kuwasaidia kuongeza juhudi za ubunifu kkatika kuleta ajira.
Kulingana na Fikirini, mpango huo utasaidia katika kubuni nafasi nyingi za ajira katika taifa ambalo nafasi hizo zimekuwa finyu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kongamano la mbinu za kuwasaidia vijana kuwa wakakamavu, ambalo limeandaliwa na mashirika ya Partnership for African Social and Governance Research (PASGR) na Mastercard Foundation, Fikirini amesema vijana wana nafasi za kutafuta mbinu za kukabiliana na changamoto zinazoikumba dunia na hivyo serikali itahakikisha wanahusishwa kikamilfiu katika ubunifu.
Amefichua kuwa serikali iliunga mkono juhudi za vijana 306 wabunifu, 266 nafasi za ubunifu, 250 mashirika katika mwaka wa kifedha wa 2024/25.
Naye seneta wa Homabay Moses Kajwang anasema serikali inafaa kuweka mbinu zitakazohakikisha kunakuwa na ushindani wa kutafuta vijana kwa nafasi za ajira badala ya vijana kupambana kujitafutia ajira.
Vijana waliohudhuria kongamano hilo sasa wanasema licha ya kuwepo changamoto za kupata ajira, ni vyema kuwe na heshima na kukubaliwa katika sehemu zao za kazi wanazopata.
Cynthia Mbithe ambaye ni mlemavu anasema mara nyingi sehemu za kazi huwabagua.
Kulingana na Mophat Okinyi, wengi wa vijana wanapewa kazi ambazo hawana tajriba nazo au hata kusomea hali ambayo inafifisha mwendelezo mwema wa ajira iliyo na heshima hata kama mapato yake ni duni.
Kulingana na Mkurugenzi Mtendaji wa PASGR Prof. Fadel Ndiame, lengo ni kuelewa changamoto za vijana kupata ajira kwa kuwasikiza.
Ndiame anasema ni heri kusikiza vijana kwanza na kuweka mipangilio ya kuwatengenezea njia ya kutafuta ajira.
PASGR inalenga kutumia maoni ya wadau tofauti ikiwemo serikali na vijana kwa kwa utafiti ili kubuni mpango wa utafiti sera utakaohusisha mataifa kumi ikiwemo Kenya kwa utafiti huo.