Faith Cherotich amejizatiti na kuishindia Kenya dhahabu ya kwanza ya mita 3000 kuruka viunzi na maji kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2019,katika siku ya tano ya mashindano ya Riadha Duniani mjini Tokyo, Japan, leo jioni.
Cherotich aliye na umri wa miaka 21 amekamilisha mbio hizo huku akiweka rekodi mpya ya dakika 8 sekunde 51 .59.
Bingwa mtetezi Winfred Yavi wa Bahrain ameshinda fedha kwa dakika 8 sekunde 56.46, huku Sembo Almayew wa Ethiopia akiridhia shaba kwa dakika 8 sekunde 58.86.
Cherotich ni Mkenya wa nne kushinda dhahabu ya wanawake katika mbio hizo katika historia ya mashindano ya dunia baada ya Milcah Chemos mwaka 2013, Hyvin Kiyeng mwaka 2015 na Beatrice Chepkoech mwaka 2019.
Kenya ni ya pili kwenye msimamo wa medali kwa dhahabu 4, fedha 1 na shaba 2, nyuma ya Marekani iliyo na medali 10, dhahabu 7, fedha 1 na shaba 2.