Alien Skin atangaza ada ya matamasha ya kimataifa

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda s Patrick Mulwana maarufu kama Alien Skin ametangaza ada ambayo atakuwa analipisha ili kutumbuiza kwenye matamasha ughaibuni.

Akizungumza katika mahojiano mwanamuziki huyo alisema kwamba atadai malipo ya Dola milioni moja za Marekani kwa kila tamasha la ughaibuni.

Alien Skin anasema kwamba amejitahidi sana kufikia kiwango alichofikia kama msanii na sasa anajiona anastahiki kuwa kwenye jukwaa moja na wakali wa muziki ulimwenguni.

Msanii huyo alimtaja msanii mwenza wa Nigeria Burna Boy ambaye alisema kwa sasa analipisha dola laki 5 kutumbuiza kimataifa lakini yake itakuwa mara mbili ya hiyo.

Alishangaa kwamba hata wasanii wenzake wa Uganda ambao humkejeli hawajafikia kiwango chake.

Wakati huo huo Alien Skin ametangaza kwamba alikuwa amepanga ziara ya Uingereza mwaka huu lakini akaamua kuiahirisha hadi mwaka ujao wa 2026, kutokana na ukweli kwamba sasa ni wakati wa siasa nchini Uganda.

Anaamini kwamba raia wa Uganda wanaoishi ughaibuni ni sehemu muhimu ya siasa za nchi hiyo na ndio walengwa wake kwenye ziara hiyo na ni muhimu awape muda hadi siasa zikamilike.

Uganda inapanga kuandaa uchaguzi mkuu Januari 2026 na kwa sasa kampeni zinaendelea.

Share This Article