Wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma kote nchini wametekeleza vitisho vyao kwa kuanza mgomo ili kuishinikiza serikali kuwalipa malimbikizi ya mshahara wao na pia kutekeleza Mkataba wa Maelewano (CBA) wa mwaka 2021-2025.
Wanasema hawatarejea kazini kamwe ngo! hadi hela zitikise akaunti zao.
Hata ahadi ya Waziri wa Elimu Julius Ogamba kwamba serikali imetoa shilingi bilioni 2.5 za kuwalipa katika awamu ya pili ya utekelezaji wa CBA ya mwaka 2021-2025 haikuwashawishi kusitisha mgomo wao.
Wanasema ahadi ya deni ni kulipa, na serikali imekawia mno kuwalipa deni lao kiasi kwamba kamwe hawatasikiliza simulizi za serikali bila vitendo.
Mjini Bungoma, wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Kibabii waliungana na wenzao nchini kushinikiza kutekelezwa kwa mkataba wao na serikali, wakisema kuwa hawatarejea darasani hadi watakaposhughulikiwa.
Wakiongozwa na Katibu Mkuu wa UASU tawi la Kibabii Nyukuri Barasa ,wanasema kuwa wamekuwa wakidanganywa na serikali kuu na kwamba CBA ya mwaka 2025-2029 haijaafikiwa na wamesalia kuhangaika kumudu maisha yao.
Aidha, wafanyakazi wa chuo hicho chini ya chama cha Kenya University Staff Union, KUSU, wakingozwa na mwenyekiti Augustine Ngome wameuangana na wahadhiri kushinikiza matakwa yao huku ratiba ya masomo chuno ikivurugika.
Katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro (MMUST) mjini Kakamega, wahadhiri waliandamana na kusitisha shughuli zote za masomo chuoni humo.
Wote hao walishinikiza kuanza kwa mazungumzo ya mkataba mpya wa makubaliano wa mwaka 2025-2029 huku pia wanataka mkataba wa awali wa 2017-2021 utekelezwe kikamilifu.
Wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali, maandamano yao yaliongozwa na mwenyekiti wa chama cha wahadhiri (UASU) tawi la MMUST, Ronald Wamalwa, pamoja na mwakilishi wa chama cha wafanyakazi wa vyuo vikuu (KUSU), Gregory Izanga.
Viongozi hao wamesisitiza kuwa hawatarejea kazini hadi matakwa yao yashughulikiwe.
Wahadhiri na wafanyakazi hao wanailaumu serikali kwa kile wanachodai kama ahadi za mara kwa mara zisizotekelezwa kuhusu nyongeza ya mishahara na marupurupu yao.
Hali ilikuwa vivyo hivyo katika vyuo vikuu vya umma kote nchini huku kaulimbiu ya wahadhiri wao ikiwa moja: hakuna pesa, hakuna kurejea kazini.
Taarifa hii imechangiwa na Josephat Doe na Carolyn Necheza