Wafanyakazi wa vyuo vikuu vya umma waanza mgomo

Dismas Otuke
1 Min Read

Wafanyakazi katika vyuo vikuu vya umma kote nchini wameanza mgomo mapema leo na kusambaratisha huduma, wakitaka walipwe malimbikizi ya mishahara na marupurupu pamoja na utekelezaji wa nyongeza mpya za mishahara.

Vyama vitatu vinavyowakilisha wafanyikazi hao – Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu (UASU), Chama cha Wafanyikazi wa Vyuo Vikuu (KUSU) na Chama cha Wahudumu wa Hoteli, Taasisi za Elimu, Hospitali na Wafanyikazi Husika (KUDHEIHA) – vimesimama tisti kuwa kamwe wanachama wao hawatarejea kazini hadi serikali itimize matakwa yao.

Ilani ya mgomo wa wafanyikazi kupitia kwa vyama hivyo vitatu iliyokuwa imetolewa tarehe 9 mwezi huu ilikamilika jana.

Wafanyikazi hao wanasema Serikali ilikosa kutimiza ahadi ya kulipa malimbikizi ya mishahara na marupurupu yao yote jinsi walivyokubaliana kufikia mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.

Mgomo huu unajiri siku chache baada ya Rais William Ruto kukutana na walimu kote nchini katika Ikulu ya Nairobi, akiwaahidi kuimarisha maslahi yao, ikiwemo kutengewa asilimia 20 ya nyumba za gharama nafuu.

Aidha, mgomo huo unajiri chini ya majuma matatu tangu wanafunzi wa mwaka wa kwanza kuripoti vyuoni.

Share This Article