Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara Yanga wameendeleza ubabe dhidi ya watani wa jadi Simba baada ya kuwalaza bao moja kwa bila Jumanne jioni kwenye mchuano wa kuwania taji la Ngao ya Jamii.
Mechi hiyo ilisakatwa katika uwanja wa kitaifa wa Benjamin Mkapa ilishuhudia Yanga wakipata bao la ushindi likipachwa kimiani na Pacome Zouzoua mwanzoni mwa kipindi cha pili.
Pambano la ngao ya Jamii hutangulia msimu mpya wa Ligi kuu Tanzania inayotarajiwa kung’oa nanga kesho Jumatano kwa mechi mbili huku michuano mingine ikisakatwa mwishoni mwa juma.
Kinondoni MC itaana msimu nyumbani dhidi ya Dodoma Jiji kesho huku Tanzania Prisons wakianza msimu safarini dhidi ya Coastal Union.
Yanga watafungua msimu Septemba 24 dhidi ya Pamba huku Simba wakianza nyumbani dhidi Fountain Gate tarehe 25.