Sekta ya elimu inakodolea janga lingine baada ya wafanyakazi wa vyuo vikuu, wakiwemo wahadhiri, kutangaza kuwa wataanza mgomo wao kesho Jumatano.
Hatua hiyo huenda ikalemaza masomo katika vyuo vikuu vingi vya umma, siku chache baada ya vyuo hivyo kurejelea masomo.
Wafanyakazi hao wanashinikiza serikali kuwalipa malimbikizi ya mshahara wa shilingi bilioni 2.73 na marupurupu ya kuanzia mwaka 2021.
Mgomo umeitishwa na chama cha UASU, kile cha wafanyakazi wa vyuo vikuu nchini Kenya (KUSU) pamoja na kile cha (KUDHEIHA).
Vyama hivyo vikisema vimeazimia kususia kazi baada ya kumalizika kwa makataa ya kuitaka serikali kuwalipa malimbikizi yao leo Jumanne.
Si hayo tu, wahadhiri pia wanashinikiza utekelezaji kamili wa mkataba wa makubaliano wa mwaka 2021-2025.
Katika juhudi za dakika za mwisho za kuepusha mgomo huo, Waziri wa Elimu Julius Ogamba ameahidi kuwa wafanyakazi hao watalipwa fedha zao kufikia mwishoni mwa mwezi huu.
Haijulikani ikiwa ahadi hiyo inaweza kuwashawishi wafanyakazi hao kufutilia mbali mgomo wao ikiwa imesalia saa chache tu kabla ya kuanza kwa mgomo huo.