Mahakama Kuu ya Milimani jijini Nairobi imetoa kibali cha kukamatwa kwa raia wa Uingereza anayeshukiwa kutekeleza mauaji ya mwanamke mmoja mjini Nanyuki, kaunti ya Laikipia mwaka 2012.
Jaji Alexander Muteti ametenga Oktoba 21, 2025, kuwa siku ya kusikilizwa kwa kesi hiyo kwa nia ya kuthibitisha iwapo kibali hico kitakuwa kimetekelezwa.
Raia huyo wa Uingereza anayeaminika kuwa mwanajeshi, anadaiwa kumuua Agnes Wanjiru Wanjiku katika hoteli moja mjini Nanyuki, kaunti ya Laikipia mwaka 2012.
Mwili wa Wanjiru uliokuwa uchi ulipatikana kwenye tanki la maji taka katika hoteli ya Lion’s Court huko Nanyuki, miezi miwili baada yake kutoweka.
Wanjiru aliingia kwenye hoteli hiyo na wanajeshi wa Uingereza wa kikosi cha ‘Duke of Lancaster’ na hakuonekana baada ya hapo.
Kesi yake ilikosa kuendelea kwa muda hadi mwaka 2021 wakati mazungumzo kati ya wanajeshi wa kikosi hicho kwenye mitandao ya kijamii wakidhihaki kifo cha Wanjiru yalivujishwa.
Mawasiliano ya maafisa hao wa ulinzi yaliangaziwa na vyombo vya habari huko Uingereza na kusababisha kufunguliwa tena kwa kesi ya mauaji ya Wanjiru aliyekuwa wa umri wa miaka 21 wakati huo.
Mwaka 2023, uchunguzi mpana kuhusu madai ya unyanyasaji na Jeshi la Uingereza ulizinduliwa.
Aprili 2025, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, John Healey alikutana na watu wa familia ya marehemu Agnes Wanjiru, akitoa pole zake na kuahidi kuendeleza msaada wa serikali ya Uingereza kwa wachunguzi wa Kenya.
Tarehe 13 Agosti 2025, Kamati ya Ulinzi, Ujasusi na Mahusiano ya Kigeni ya Kenya iliwataja maafisa waandamizi kutoka Kikosi cha Mafunzo cha Jeshi la Uingereza nchini Kenya (BATUK) kuwa ‘mashahidi wa uhasama’ kwa kukosa kuhudhuria kikao cha bunge.
Ni Waziri wa Ulinzi wa Kenya, Soipan Tuya, na Katibu wake wa Kudumu pekee waliohudhuria.
Kamati hiyo iliamini kuwa BATUK waliepuka kikao hicho makusudi na ikaonya kuhusu madhara makubwa, kama vile maagizo ya kukamatwa, faini au kuendeleza uchunguzi bila wao.