Serikali ya kaunti ya Meru na ile ya kitaifa zimetangaza mipango ya kujenga ikulu ndogo kama sehemu ya mpango mkubwa wa kuhakikisha mji wa Meru unapatiwa hadhi ya jiji.
Mradi huo uliopendekezwa ni sehemu ya miradi mingine ya kimkakati inayolenga kuafiki sera ya kitaifa ya maendeleo ya miji.
Katika mkutano wa ngazi za juu na katibu wa idara ya misitu Gitonga Mugambi, viongozi wa kaunti waliorodhesha miradi muhimu kama uwanja wa ndege, uwanja wa gofu na kutengwa kwa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa ikulu hiyo ndogo.
Maafisa hao wa kaunti wanahisi kwamba miradi hiyo itakuwa nguzo muhimu katika kubadili mji wa Meru na kuufanya wa kisasa huku ikiimarisha ukuaji wa uchumi na uwekezaji katika eneo hilo.
Gavana wa kaunti ya Meru Mutuma M’Ethingia aliangazia haja ya kuwianisha miundo msingi na mipango endelevu, akisisitiza kwamba mipango hiyo itaboresha mvuto wa mji wa Meru bila kuhatarisha mazingira na utamaduni.