Bingwa wa dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 Edmund Serem ameishindia Kenya nishani ya shaba ya mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji katika mashindano ya Riadha Ulimwenguni leo Jumatatu jioni.
Serem amekamilisha mbio hizo kwa muda wa dakika 8 sekunde 34.56, ikiwa medali ya kwanza katika mbio za watu wazima.
Gordie Bimmish wa New Zealand ndiye bingwa mpya wa shindano hilo baada ya kutumia dakika 8 sekunde 33.88, akimlemea bingwa wa mwaka 2023 Soufiane El Bakkali wa Morocco, aliyeshinda fedha kwa dakika 8 sekunde 33.95.
Matokeo hayo yanaiacha Kenya ikiendeleza ukame wa dhahabu ya mbio hizo, tangu Consenslus Kipruto aliposhinda dhahabu mwaka 2019 mjini Doha, Qatar, akimrithi Ezekiel Kemboi aliyekuwa ameshinda dhahabu nne za mbio hizo.