KDF yatangaza usajili wa makurutu Oktoba

Marion Bosire
1 Min Read

Jeshi la ulinzi la Kenya KDF, limetangaza kwamba litaandaa zoezi la usajili wa makurutu kote nchini mwezi ujao wa Oktoba.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumapili, jeshi hilo lilifafanua kwamba usajili huo utahusisha vitengo mbali mbali kama vile maafisa wa majukumu ya jumla, Makadeti wa kawaida na walio na shahada, wataalamu, makurutu wa huduma jumla, maafisa wenye ujuzi wa kazi za mikono na makonstebo wa ulinzi.

Wanaotaka kujiunga na jeshi wameshauriwa kuzuru tovuti ya usajili ya KDF na kuweka maombi huko kabla ya Oktoba 12. Watakaochaguliwa watafahamishwa kupitia matangazo kwenye gazeti kati ya Oktoba 21 na 24.

KDF baadaye itatuma maafisa wa usajili kutoka vitengo vyake vitatu nyanjani kutathmini watakaokuwa wamechaguliwa mtandaoni.

Wanaotamani kuwa wanajeshi na wanapania kutuma maombi wanahitajika kuwa raia wa Kenya, wawe na vitambulisho vya kitaifa, nambari ya utambuzi ya shirika la ukusanyaji ushuru nchini KRA na vyeti vya masomo.

Jeshi hilo limetoa orodha kamili ya vituo vitakavyotumika kutathmini makurutu watakaokuwa wamechaguliwa mtandaoni kupitia magazeti ya leo.

Share This Article