Hilda Effiong Bassey maarufu kama Hilda Baci ni mpishi maarufu wa asili ya Nigeria ambaye ameweka historia ya kupika sufuria kubwa zaidi la wali aina ya Jollof duniani.
Baci aliandaa mapishi hayo katika uwanja wa hoteli ya Eko jijini Lagos nchini Nigeria Septemba 12, 2025 kwa lengo la kuvunja rekodi ya dunia ya Guinness kwa mara nyingine.
Iliarifiwa kwamba sufuria la zaidi ya lita elfu 22, alilotumia mpishi huyo liliundwa kwa muda wa miezi mitatu na kugharimu utaalamu wa watu wapatao 300.
Kilo elfu nne za wali, katoni 500 za ‘tomato paste’, kilo 600 za vitunguu na kilo 750 za mafuta ya kupikia ndivyo baadhi ya viungo vilivyotumika katika mapishi hayo.
Mpishi huyo alitumia muda wa saa tisa kukamilisha mapishi akisaidiwa na wapishi wengine 10 na kisha kupakua kwenye vibakuli vidogo na kugawia watu zaidi ya elfu 30 waliokusanyika kushuhudia tukio hilo.
Juhudi za mpishi huyo zilitambuliwa na wengi akiwemo Waziri wa Habari na Mwelekeo wa Kitaifa wa Nigeria, Mohammed Idris, aliyempongeza Hilda, akisema jaribio lake linaonyesha ubunifu na uwezo wa Vijana wa Nigeria katika kuleta maendeleo na kutambulika kimataifa.
Hilda Baci sasa anasubiri uthibitisho rasmi kutoka Guinness World Records ili kuidhinisha jaribio lake kama rekodi mpya ya dunia.
Hii ni mara ya pili kwa Hilda kujaribu kuvunja rekodi, baada ya kufanikiwa kupika kwa muda mrefu zaidi duniani kama mtu binafsi mwaka 2023.