Mshukiwa wa mauaji ya Charlie Kirk akamatwa

Marion Bosire
2 Min Read

Polisi nchini Marekani walimkamata mshukiwa mkuu wa mauaji ya mwanaharakati Charlie Kirk baada ya msako uliodumu takriban masaa 33.

Mshukiwa huyo kwa jina Tyler Robinson wa umri wa miaka 22 mkazi wa eneo la Utah alikamatwa Alhamisi jioni kulingana na saa za Marekani na Rais Trump alikuwa wa kwanza kutangaza hilo.

Kirk alipigwa risasi shingoni akiwa jukwaani katika hafla iliyokuwa ikiandaliwa katika chuo kikuu mapema wiki hii.

Inaripotiwa kwamba babake Tyler ndiye alimlazimisha ajisalimishe baada ya yake kukiri kwake kwamba yeye ndiye alitekeleza kitendo hicho cha unyama.

Awali Tyler alikuwa amekataa kujisalimisha akisema heri kufa kuliko kujisalimisha lakini baada ya ushawishi kutoka kwa mhubiri wa vijana akabadili mawazo.

Mhubiri huyo ambaye pia anafanya kazi kama mlinzi katika mahakama na baba ya kijana huyo waliwapigia simu polisi Alhamisi saa nne usiku saa za Marekani ambao walifika na kumkamata.

Gavana wa jimbo la Utah, Spencer Cox salisema kwamba picha zilizonaswa na kamera za ulinzi zilimwonyesha Tyler akifika katika chuo kikuu cha Utah Valley masaa manne kabla ya ufyatuaji huo wa risasi.

Wakati wa kukamatwa kwake Tyler alikuwa bado amevaa mavazi aliyoonekana nayo kwenye video hizo na watu wa familia yake waliohojiwa walisema katika siku za hivi karibuni alikuwa ameingilia masuala ya siasa sana.

Mshukiwa huyo anadaiwa kuzungumza kuhusu ujio wa Kirk katika chuo kikuu cha Utah siku za awali na alimtaja kuwa mtu aliyejawa na chuki na ambaye anaeneza chuki.

Jamaa ambaye anaishi na Tyler pia alisaidia maafisa wa usalama kupata jumbe za mawasiliano kuhusu namna ya kupata bunduki aliyotumia na mahali ambapo angeibwaga baada ya matumizi.

Maganda ya risasi yaliyopatikana karibu na bunduki hiyo yalikuwa na maandishi ya chuki kwa Kirk pamoja na ya kumpigia kwaheri.

Share This Article