Tumikieni taifa kwa unyenyekevu, Mudavadi awasihi Makamishna wa IEBC

Martin Mwanje
1 Min Read
Waziri Musalia Mudavadi akiwa na Makamishna wa IEBC ofisini mwake

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC Erastus Ethekon leo Ijumaa amewaongoza makamishna wa tume hiyo katika kumtembelea Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ofisini mwake.

Wakati wa mkutano wao, Mudavadi aliwapongeza makamishna wao kwa kuteuliwa kwenye wadhifa huo, uteuzi ambao alisema ni fadhila kubwa.

Aidha, Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje aliwataka Ethekon na timu yake kuhudumu kwa unyenyekevu, uthabiti na uwazi.

Ethekon aliahidi kuhakikisha wanaendesha chaguzi za wazi ili kurejesha imani ya Wakenya kwa tume hiyo.

Ikiwa wataweza kufanya hivyo au la itabainika Novemba 27 pale tume hiyo mpya itakapoendesha jumla ya chaguzi ndogo 24 katika maeneo mbalimbali nchini.

IEBC iko mbioni kufanya maandalizi ya chaguzi hizo zitakazoandaliwa katika maeneo bunge kama vile Malava, Ugunja, na Mbeere Kaskazini, na pia wadi kadhaa.

Kiti cha Malava kilisalia wazi kufuatia kifo cha mbunge wa eneo hilo Malulu Injendi huku maeneo ya Ugunja na Mbeere Kaskazini yakikosa mjumbe baada ya wabunge Opiyo Wandayi na Geoffrey Ruku kuteuliwa kuwa mawaziri mtawalia.

 

 

Share This Article