Jopo la fidia lataka maagizo ya kusitisha shughuli zake kuondolewa

Mahakama Kuu ya Kerugoya ilitoa maagizo ya kusitisha shughuli za jopo hilo Jumatatu wiki hii baada ya mwanasheria Levi Munyeri kuwasilisha kesi katika mahakama hiyo kupinga uhalali wa jopo hilo. 

Martin Mwanje
2 Min Read
Jopo la fidia baada ya uapisho ulioongozwa na Msajili Mkuu wa Mahakama Winfridah Mokaya

Jopo la fidia kwa waathiriwa wa maandamano tangu mwaka 2017 limewasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Kerugoya likiitaka kuondoa maagizo ya kulizuia kuendelea na shughuli zake. 

Mahakama hiyo ilitoa maagizo hayo Jumatatu wiki hii baada ya mwanasheria Levi Munyeri kuwasilisha kesi katika mahakama hiyo kupinga uhalali wa jopo hilo.

“Jopo kwa kutii maagizo ya mahakama limesitisha shughuli zake na litaendelea kuheshimu maagizo hayo hadi lipate maelekezo zaidi kutoka kwa mahakama,” limesema jopo hilo kwenye taarifa.

Rais William Ruto mwishoni mwa mwezi jana aliteua jopo la watu 18 kusimamia mchakato wa kuwalipa fidia waathiriwa wa maandamano katika kipindi cha miaka 8 iliyopita.

Prof. Makau Mutua ambaye ni mshauri wa Rais kuhusu masuala ya kikatiba aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa jopo hilo huku Rais wa Chama cha Wanasheria nchini, LSK Faith Odhiambo akiteuliwa kuwa naibu mwenyekiti.

Kwenye taarifa leo Alhamisi, Odhiambo amesema anatafuta ushauri kuhusiana na wajibu wake kwenye jopo hilo kabla ya kuamua mwelekeo atakaochukua.

Odhiambo amestahimili mashambulizi makali kutoka kwa baadhi ya Wakenya kwa kuridhia kuhudumu katika jopo hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Amnesty International Kenya Irungu Houghton pia ametangaza kujiondoa kwenye jopo hilo baada ya mahakama kusitisha utendaji kazi wake.

Hata hivyo, Irungu amesisitiza umuhimu wa waathiriwa wa maandamano kutendewa haki.

Share This Article