Wizara ya Leba imetangaza nafasi za ajira ughaibuni kwa waendeshaji pikipiki maarufu kama ‘bodaboda’ katika Milki za Kiarabu.
Kulingana na Waziri wa Leba Dkt Alfred Mutua kupitia kwa mtandao wa X, Wakenya wote walio na ujuzi unaohitajika wanatakiwa kufika kwa mahojiano yatakayoanza leo, Septemba 11, hadi Jumamosi hii katika chuo cha kitaifa cha masomo ya Viwandani (NITA), eneo la Athi River kati ya saa mbili asubuhi na saa kumi na moja jioni.
Hata hivyo Waziri Mutua amefichua kuwa kazi hizo ni kwa waendeshaji pikipiki wa kiume pekee walio na umri kati ya 21 na 38, na lazima watahiniwa wote watafanyiwa majaribio ya kuendesha pikipiki, kuwa na ufahamu wa Kiingereza na wawe na uwezo wa kutumia Google Maps.
Watakaofaulu kupata kazi hizo watapokea mshahara wa kati ya shilingi 73,000 na 87,000 kwa kila mwezi.