Mwanamuziki wa Uganda Ali Buken maarufu kama Nubian Li jana alitiwa mbaroni na maafisa wa polisi muda mfupi baada yake kuidhinishwa rasmi na tume ya uchaguzi kuwania wadhifa wa Meya eneo la Nakawa.
Kisa hicho kilitokea jana nje ya afisi za tume ya uchaguzi ya Uganda tawi la Ntinda.
Msemaji wa chama cha upinzani cha National Unity Platform – NUP na ambaye pia ni kiongozi wa upinzani bungeni Joel Ssenyonyi alitoa taarifa kuhusu tukio hilo jana mitandaoni.
Li ambaye ni rafiki wa muda mrefu wa mwanamuziki mwenza Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine, pia ni mwanachama wa chama anachokiongoza Wine cha NUP.
Muda mfupi baada ya tukio hilo, Li kupitia akaunti yake ya mtandao wa X alitangaza kwamba polisi waliomkamata walimwachilia bila kumchukulia hatua yoyote.
“Asante nyote marafiki kwa hisia na jumbe za kudhihirisha umoja. Nilikamatwa nje ya afisi za tume ya uchaguzi punde baada ya kuteuliwa kuwania” alisema msanii huyo na mwanasiasa kwa ujumbe wake.
Aliendelea kusema, “Baada ya kuzungushwa kwa muda nilipelekwa nyumbani. Walidai kwamba nilikuwa ninapanga maandamano.”
Kukamatwa kwa Li kulijiri baada ya msemaji wa chama cha NUP Alex Waiswa Mufumbiro kukamatwa juzi alasiri nje ya mahakama ya hakimu ya Kawempe.
Haya yanajiri wakati ambapo taifa hilo la Afrika mashariki linajiandaa kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kuandaliwa Januari mwakani.