Huku shule zikiendelea kukabiliwa na changamoto ya fedha na wanafunzi kutumwa nyumbani kutafuta karo katika kaunti ya Trans Nzoia, zaidi ya wanafunzi 8,000 kutoka jamii isiyojiweza na wanaosoma katika shule za kutwa wamenufaika na basari za masomo kutoka kwa mfuko wa basari ya elimu wa kaunti hiyo.
Akihutubu wakati wa utoaji wa hundi kwa wanafunzi katika wadi za Kiminini, Sikhendu, Makutano na Endebess, Waziri wa Elimu wa kaunti ya Trans Nzoia Janerose Nasimiyu Mutama amekosoa hatua ya serikali kuu kutoruhusu kaunti kufadhili elimu kwa shule za upili, vyuo vya kati na vyuo vikuu akiongeza kuwa hatua hiyo ni hujuma kwa wanafunzi wa wazazi kutoka jamii zisizojiweza.
Aidha, Mutama ametoa wito kwa Wizara ya Elimu nchini kuharakisha utoaji wa fedha za kufadhili elimu akisema walimu wakuu wanapitia hali ngumu ya kuwahudumia wanafunzi shuleni bila fedha akisema fedha zinazotolewa na serikali ya kaunti hazitoshi.
Wakati huo huo, Mutama amesema wizara yake kupitia kwa maafisa wake imejitolea kupeleka hundi hizo moja kwa moja shuleni na kuwapa wanafunzi wanaolengwa ili kuhakikisha uwazi na wanafunzi wanafaidi msaada huo kinyume cha hapo awali.