Wafanyakazi wa chuo kikuu cha Moi jana Jumanne walitangaza kusitisha mgomo uliodumu kwa majuma matatu, baada ya kuafikiana na wasimamizi chuoni humo.
Viongozi wa chama cha wafanyakazi wa vyuo vikuu nchini (UASU), wakiongozwa na Katibu Mkuu Dkt. Constantine Wasonga, walitangaza kufutilia mbali mgomo huo baada ya kufanya kikao na mwenyenyekiti wa chuo hicho Prof. Noah Midambo katika makao makuu ya chuo hicho mjini Eldoret.
Mgomo huo ulioanza Agosti 20 mwaka huu ulikuwa umedumu kwa majuma matatu huku masomo yakiathirika vibaya.
Miongoni mwa matakwa ya wafanyakazi hao ni pamoja na ulipaji malimbikizi ya mishahara ya shilingi bilioni 9.7, utekelezaji wa nyongeza mpya ya mshahara ya mwaka 2017-2021, kurejesha bima ya matibabu na kuwasilishwa kwa makato yote ya mishahara ya wafanyakazi kwa taasisi lengwa.