Seneti yafafanua kuhusu mswada wa marekebisho ya katiba

Marion Bosire
2 Min Read

Bunge la Seneti nchini limefafanua kuhusu yaliyomo kwenye mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2025.

Kupitia akaunti rasmi ya mtandao wa X, bunge hilo limeelezea yaliyomo kwenye mswada huo huku likitaja nakala iliyosambazwa awali mitandaoni kuwa ghushi.

Seneti imekanusha madai kwamba mswada huo unalenga kuongeza muhula wa kuhudumu wa Rais na viongozi wengine waliochaguliwa kutoka miaka mitano hadi miaka saba.

Bunge hilo likirejelea ujumbe uliochapishwa na mwanaharakati Hussein Khalid uliotishia kwamba Wakenya watarejelea maandamano kufuatia yaliyopendekezwa kwenye mswada huo huku akikanusha habari hizo.

“Ujumbe huu sio sahihi. Mtazamo wa mswada rasmi wa marekebisho ya katiba mwaka 2025 unaonyesha kwamba yanayosemwa mitandaoni sio ya kweli.” ulisema ujumbe wa Seneti.

Bunge hilo lilisema kwamba hakuna kipengele kinachopendekeza kuongezwa kwa muhula wa viongozi wala kuundwa kwa wadhifa wa waziri mkuu atakayeteuliwa na Rais.

Kulingana na ufafanuzi huo, mswada huo unalenga kuimarisha ugatuzi na jukumu la bunge la Seneti kwa kulifanya bunge hilo kuwa sawa na bunge la kitaifa ili kuhakikisha kwamba miswada ni lazima ipitishwe na mabunge yote mawili.

Unapendekeza pia kuimarishwa kwa uwezo wa bunge la Seneti katika uangalizi wa matumizi ya pesa za serikali kwa kulipa mamlaka ya kuhusika katika uundaji wa bajeti na katika kuidhinisha uteuzi wa maafisa muhimu wa serikali kama msimamizi wa bajeti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali.

Suala lingine linalopendekezwa na mswada huo ni ulinzi wa mabunge ya kaunti kupitia kuanzishwa kwa hazina ya mabunge ya kaunti inayolindwa na katiba ili kuhakikisha uhuru wa kifedha wa mabunge hayo.

“Ni muhimu kusoma na kuhakiki jumbe kabla ya kusambaza” ilishauri Seneti.

Share This Article