Busta Rhymes afungua tuzo ya heshima ya Rock The Bells Visionary

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki nyota wa muda mrefu wa mtindo wa hip-hop Busta Rhymes alikiwasha katika jukwaa la Tuzo za video za muziki za MTV ambapo pia alifungua kipengele cha tuzo  kilichosubiriwa kwa hamu cha heshima kilichopatiwa jina la “ROCK THE BELLS VISIONARY”.

Aliandaa onyesho lililowaacha mashabiki wakishangilia kwa kelele katika hafla hiyo ya tuzo.

Busta alipakulia waliokuwa wakihudhuria mchanganyiko wa nyimbo zake za zamani kutoka “Gimme Some More” hadi “Break Ya Neck” na kuziunganisha kwa ustadi na wimbo mpya mzito uliotayarishwa na Hit-Boy.

Mtindo wake wa kufoka maneno kwa kasi na uwepo wake wa nguvu jukwaani ulithibitisha tena kwa nini bado anahesabiwa kati ya wasanii wa hip-hop wenye mvuto mkubwa zaidi.

Tuzo ya heshima ya ROCK THE BELLS VISIONARY, iliyoratibiwa kwa ushirikiano na jukwaa la LL COOL J, inatambua wasanii waliobadilisha utamaduni na kuvuka mipaka ya muziki.

Busta, anayejulikana kwa video zake za kipekee na haiba isiyo na mfano, ameandikisha historia ya kuwa msanii wa kwanza kabisa kutunukiwa heshima hiyo.

Nyota wenzake kama Missy Elliott, Kendrick Lamar na Doja Cat pia walimwonyesha heshima ya kipekee kwa kusimama wakati akipokezwa tuzo yake.

“Hip-hop sio muziki tu, ni harakati, ni mtazamo wa maisha” alisema Busta kwa sauti kali ndani ya ukumbi wa Prudential Center akiongeza “Bado tunavunja mipaka”.

Onyesho hilo liliashiria tukio la kihistoria: gwiji hai anayejenga daraja kati ya enzi ya dhahabu ya hip-hop na kizazi kijacho. Na ujumbe ulikuwa wazi kabisa Busta Rhymes bado yuko mstari wa mbele.

Share This Article