Maafisa wa sheria Afrika Mashariki wakutana kwa mafunzo ya kukabili biashara haramu ya wanyamapori

Marion Bosire
2 Min Read

Maafisa wa utekelezaji wa sheria kutoka Kenya, Uganda na Tanzania wanakutana jijini Nairobi kwa warsha ya kikanda ya ngazi ya juu yenye lengo la kuimarisha juhudi za kukabiliana na biashara haramu ya wanyamapori Afrika Mashariki.

Warsha hiyo ya siku tatu, inayoendelea katika Hoteli ya Golden Tulip, ilifunguliwa rasmi na Ibrahim Jillo mkurugenzi wa afisi ya kituo kikuu cha polisi cha kimataifa Nairobi.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Jillo alisisitiza haja ya haraka ya ushirikiano wa kikanda akisema, “Kulinda wanyamapori wetu ni jukumu la pamoja. Sio kazi ya taasisi moja au taifa moja, ni dhamira yetu sote.”

Warsha hii imeandaliwa na shirika la TRAFFIC International East Africa, shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na kuhakikisha biashara ya wanyamapori ni halali na endelevu.

Warsha hii imewaleta pamoja maafisa wa polisi, waendesha mashtaka, maafisa wa mahakama na wataalamu wa masuala ya wanyamapori.

Lengo kuu ni kuimarisha ushirikiano wa mipakani na kuboresha usambazaji wa taarifa kijasusi kati ya mashirika ya utekelezaji sheria.

Jillo alieleza kuwa biashara haramu ya wanyamapori sio tu tishio kwa mazingira bali pia ni hatari kwa usalama wa kikanda, utawala bora na maisha ya jamii zinazotegemea rasilimali za asili.

Mikala Lauridsen, mkurugenzi wa shirika la TRAFFIC East Africa alikaribisha washiriki na kueleza matumaini kwamba warsha hii itachochea ushirikiano madhubuti na utekelezaji bora wa sheria.

Miongoni mwa wageni mashuhuri waliokuwepo ni Jaji Mstaafu Robert Makaramba kutoka Tanzania na Stephen Okiror kutoka Wizara ya Rasilimali Asili ya Uganda, wakionyesha umuhimu wa juhudi za pamoja kulinda wanyamapori wa Afrika Mashariki.

Share This Article