Kesi dhidi ya Lissu kuendelea leo

Marion Bosire
2 Min Read
Tundu Lissu, Kiongozi CHADEMA

Mwenyekiti wa chama cha CHADEMA nchini Tanzania Tundu Lissu atarejea mahakamani leo kwa ajili ya kuendelea kwa kesi inayomkabili ya uhaini iliyoanza jana na kikao cha maandalizi.

Mahakama ilitoa uamuzi wa kuahirisha kesi hiyo hadi leo Septemba 9, 2025, kufuatia ombi la Lissu la kupatiwa muda wa kudurusu nyaraka za mashauri.

Lissu aliambia mahakama kwamba nyaraka alizopokea akiwa gerezani zilikuwa tofauti na zile alizokabidhiwa na Mahakama Kuu, akidai kwamba tofauti hizo zinaweza kuathiri mwenendo wa kesi.

Aidha, Lissu kupitia mawakili wake aliwasilisha mapingamizi mawili katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo jijini Dar es Salaam, mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Nduguru.

Anapinga mwenendo wa kesi hiyo kufuatia hatua ya kuhamishwa kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hadi Mahakama Kuu bila kufuata taratibu stahiki za kisheria.

Nje ya Mahakama, Wakili Daktari Rugemeleza Nshala alieleza kuwa mapingamizi hayo yamejikita katika hoja za msingi za kisheria, ikiwemo ukosefu wa mamlaka ya Mahakama ya Kisutu kuendesha kesi hiyo.

Kwa mujibu wa sheria, iwapo mahakama ya wilaya au hakimu mkazi haina mamlaka juu ya mashtaka yanayomkabili mshtakiwa, kesi hiyo inafaa kupelekwa moja kwa moja Mahakama Kuu.

Daktari Nshala aliongeza kuwa mteja wake pia anapinga mchakato mzima uliofanyika kuanzia wilayani Mbinga mwezi Aprili mwaka 2024 hadi kufikishwa jijini Dar es Salaam mwezi Aprili mwaka 2025, akidai ulikuwa kinyume na taratibu za kisheria.

Share This Article