Magavana wana siku 21 kusuluhisha changamoto chungu nzima zinazoikumba sekta ya afya nchini la sivyo wakumbane na mgomo wa wahudumu wa afya utakaosambaratisha utoaji huduma katika kaunti zote 47 kote nchini.
Vyama 6 vya wahudumu wa afya vikiongozwa na Chama cha Maafisa wa Kliniki nchini, KUCO, vimewanyoshea Magavana kidole cha lawama kwa kuzembea kazini.
“Ikiwa Baraza la Magavana linaona kuwa wahudumu wa afya ni mzigo, wanapaswa kuunga mkono kuanzishwa kwa Tume ya Huduma za Afya – pendekezo ambalo vyama vya wahudumu wa afya viko tayari kuliunga mkono ili kupata suluhu ya kudumu kwa changamoto za kazi na migomo katika kaunti,” ilisema taarifa iliyotiwa saini na viongozi wa vyama hivyo leo Jumatatu.
“Hatua ya Magavana kuendelea kukataa mapendekezo ya mapitio ya mishahara nambari 3 na 4, na kushindwa kwao kutenga bajeti ili kuongeza mishahara ambayo ni halali, inakiuka kifungu 230 na kudhoofisha mpangokazi wa kikatiba wa kuratibu mishahara.”
Miongoni mwa mambo mengine, vyaa hivyo sasa vinataka wahudumu wote wa mpango wa upatikanaji wa afya kwa wote, UHC kupatiwa kandarasi za kudumu kufikia mwisho wa mwezi huu.
Kuajiriwa kwa wahudumu wa UHC kumeibua mivutano kati ya serikali kuu na serikali za kaunti, Magavana wakitaka mpango wa kuwaajiri wahudumu wa UHC kwa kandarasi za kudumu kusitishwa ili kupisha mashauriano zaidi.