Mahakama Kuu ya Kerugoya leo Jumatatu imetoa agizo linalozuia jopo la fidia kwa waathiriwa wa maandamano tangu mwaka 2017 dhidi ya kuanza kazi.
Hii ni hadi kesi iliyowasilishwa na mwanasheria Levi Munyeri mahakamani kupinga uhalali wa jopo hilo itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Siku chache zilizopita, Rais William Ruto aliteua jopo la watu 16 kusimamia mchakato wa kuwalipa fidia waathiriwa wa maandamano katika kipindi cha miaka 8 iliyopita.
Jopo hilo linaongozwa na Prof. Makau Mutua ambaye ni mshauri wa Rais kuhusu masuala ya kikatiba.
Naibu mwenyekiti jopo hilo ni Rais wa Chama cha Wanasheria nchini, LSK Faith Odhiambo.
Odhiambo ameshambuliwa vikali kwenye mitandao ya kijamii baada ya kukubali kuhudumu kwenye wadhifa huo, akituhumiwa kwa kukubali kufanya kazi na utawala wa Kenya Kwanza.
Awali, Munyeri alielekea mahakamani akimtaka Odhiambo kujiuzulu wadhifa wake kama Rais wa LSK baada ya kukubali kuhudumu kwenye jopo hilo.
Ni hatua ambayo imeibua mdahalo wa kisheria huku baadhi ya wanasheria wakikosoa hatua yake na wengine kuiunga mkono.