Ruto apendekeza mabadiliko katika mfumo wa kifedha ulimwenguni

Marion Bosire
2 Min Read

Katika kile kinachoonekana kuwa wito wa dharura, Rais William Ruto amependekeza mabadiliko makubwa katika taasisi za kimataifa za kifedha akionya kwamba bila hatua mwafaka, mataifa yanayokua yatasalia na madeni milele.

Kulingana naye, mataifa hayo yataishia kushindwa kushughulikia mabadiliko ya tabianchi na kuafikia maendeleo endelevu.

Akizungumza katika makala ya pili ya kongamano la Afrika-CARICOM katika afisi ya Umoja wa Mataifa mjini Addis Ababa, Ethiopia, Rais aliangazia hali kusalia ilivyo.

Ruto alisema kwamba uthabiti wa kiuchumi sio suala gumu bali ndio msingi wa maendeleo akilalamika kwamba mifumo iliyoko sasa imeshindwa kuleta mabadiliko halisi hata baada ya miaka kadhaa ya mjadala wa ulimwengu mzima.

“Mataifa ya Afrika yapatayo 21 yako katika dhiki ya madeni au katika hatari ya kuingia kwenye dhiki hiyo” aliendelea kusema Rais akiangazia jinsi kiwango cha ulipaji madeni kinazidi uwekezaji katika masuala muhimu kama afya na elimu.

Rais Ruto alipendekeza mpango wa hatua tano, akitoa wito wa kubadilishwa kwa madeni kwa njia ya haki na ufanisi, kurejeshwa haraka kwa ufadhili wa IDA na ADF, kuongezwa kwa mtaji wa benki za kimataifa za maendeleo na kuwaziwa upya kwa masharti ya shirika la kimataifa la kifedha IMF.

Kiongozi huyo wa Kenya alipendekeza pia utambuzi wa mabadiliko katika sekta ya nishati kama nguzo ya malengo ya Afrika ya kuafikia sekta ya viwanda isiyochafua mazingira.

Akitaja matokeo ya kongamano la mabadiliko ya tabianchi la mwaka 2023 la Afrika, Ruto alisisitiza kwamba muda wa maneno matupu umekwisha na mabadiliko katika benki za maendeleo ndiyo njia pekee ya ufadhili faafu.

Ruto alimalizia kwa kuhimiza umoja kati ya Afrika, mataifa ya Karibea na mataifa ya eneo la kusini kwa jumla.

Share This Article