Rais Samia asema uongozi wake ni wa vitendo

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi – CCM, amesema serikali yake haiongozwi kwa maneno bali kwa vitendo.

Alikuwa akizungumza katika mkutano wa kampeni katika mkoa wa Iringa jana Jumamosi ambapo aliongeza pia kwamba vitendo hivyo hugusa raia wa Tanzania moja kwa moja hata walio vijijini.

Kiongozi huyo alikuwa akijibu madai kwamba serikali yake si ya wanyonge akisisitiza kwamba maendeleo yaliyofanyika vijijini ndiyo tafsiri halisi ya kuwatumikia wanyonge.

“Tangu nimeanza kampeni mambo mengi yaliyokuwa yanasemwa ni yale yanayowagusa Watanzania wote hasa wale wa kule kijijini chini. Walisema hii serikali sio ya wanyonge, nikawajibu: mimi siongozi wanyonge, mimi ninaongoza Watanzania ninaotaka kuwajengea Tanzania tunayoitaka” Alisema.

Samia alitaja hatua kubwa zilizopatikana chini ya uongozi wake kama upatikanaji wa huduma za msingi vijijini na vitongojini kama vile umeme, maji safi kupitia miradi ya mabomba, ujenzi wa zahanati na vituo vya afya vyenye vifaa na vipimo vya kisasa na ujenzi wa shule bora vijijini ili watoto wapate fursa sawa na wale wa mijini.

Rais huyo aliomba wananchi waendelee kukiamini chama cha CCM na kumchagua tena ili kuhakikisha kasi hiyo ya maendeleo vijijini inaendelezwa na kuimarishwa zaidi.

Kampeni zinaendelea nchini Tanzania kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kuandaliwa mwisho wa mwezi Oktoba mwaka huu wa 2025.

Share This Article