Maporomoko ya ardhi Sudan: Pande zinazozozana zatakiwa kutoa fursa ya misaada kwa waliothirika

Martin Mwanje
1 Min Read
Picha kwa hisani ya Reuters

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mohamoud Ali Youssouf, amezitaka pande zinazozozana nchini Sudan kusitisha mapigani ili kuruhusu utoaji wa haraka wa misaada ya kibinadamu kufuatia maporomoko ya ardhi yaliyosababisha vifo vya mamia ya watu katika eneo la Marra huko Darfur.

Makundi ya waasi yanasema takriban watu elfu moja walifariki mvua kubwa iliponyesha kijiji kizima,

Vuguvugu la Ukombozi wa Sudan, ambalo linadhibiti eneo hilo, linasema maafa hayo yalitokea siku ya Jumapili baada mvua kubwa kunyesha kwa siku kadhaa katika eneo hilo.

Baadhiya waathiriwa walikuwa wamekimbia mapigano kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya waasi wa RSF huko Darfur Kaskazini, wakitafuta hifadhi milimani.

Baraza la Uhuru wa Mpito linaloongozwa na jeshi limeelelezea kusikitishwa kwake na vifo vya mamia ya watu, bila kutoa takwimu za kuthibitisha idadi kamili.

Umoja wa Mataifa unasema ripoti za ndani zinaonyesha kati ya watu 300 na 1,000 huensa wamefariki katika janga hilo.

Shirika la misaada ya kimatibabu la Madaktari Wasio na Mipaka linasema kiwango cha uharibifu bado hakijathibitishwa kikamilifu.

Maafisa wake wanafuatilia hali ilivyo katika eneo hilo kwa ushirikiano na mashirika mengine ya misaada.

Share This Article