Magavana wakosoa mfumo wa manunuzi wa serikali kuu

Martin Mwanje
2 Min Read

Hali ya vuta ni kuvute imeibuka kati ya serikali kuu na serikali za kaunti, kiini cha mvutano huo kikiwa uzinduzi wa mfumo wa manunuzi kwa njia ya elektroniki.

Mfumo huo ulipendekezwa na serikali kuu kupitia Wizara ya Fedha. Isitoshe, Waziri wa Fedha John Mbadi ameonya kuwa serikali kuu haitakubali kufanywa kwa manunuzi yoyote nje ya mfumo huo katika hatua inayolenga kuziba husan mianya ya ufisadi na ubadhirifu wa fedha serikalini.

Hata hivyo, Baraza la Magavana (CoG) likiongozwa na mwenyekiti wake Ahmed Abdullahi wametilia dosari mfumo huo wakidai utekelezaji wake uliharakishwa na hivyo kutatiza utoaji huduma muhimu kwa raia.

 

 

Wakiwahutubia wanahabari baada ya Kikao Kisicho cha Kawaida cha Baraza hilo kilichoandaliwa leo Jumatatu, Magavana hao wamesema utekelezaji wa mfumo huo ulifanyika baada ya kufanyiwa majaribio katika kaunti tatu pekee, hatua wanayosema imetatiza mno manunuzi hususan katika sekta ya afya.

Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga ni naibu mwenyekiti wa CoG. Akiwahutubia wanahabari wakati wa kikao hicho, alisema wamedhamiria kufanikisha utoaji huduma kwa raia, ila serikali kuu ni lazima iwe na hulka ya kuheshimu siyo tu mfumo wa ugatuzi bali pia ushirikiano wa kikatiba.

Magavana wakionya kuwa kamwe hawatashurutishwa kutumia mfumo huo.

Badala yake, wametoa wito wa kuisitishwa kwa utekelezaji wa mfumo huo mara moja ili kupisha, miongoni mwa mambo mengine, kufanywa kwa mashauriano zaidi kati ya pande husika.

 

 

 

 

Share This Article