Afisa mmoja wa Polisi wa Kenya anayehudumu mwenye mpango wa kimataifa wa usaidizi wa usalama unaoongozwa na Kenya nchini Haiti amefariki dunia.
Huduma ya taifa ya polisi nchini NPS imethibitisha haya na kufafanua kwamba afisa huyo alifariki katika ajali mbaya ya barabarani.
Kulingana na taarifa rasmi kutoka makao makuu ya NPS, ajali hiyo ilitokea Jumapili, Agosti 31, 2025, majira ya saa 11:00 jioni kwa saa za Haiti, sawa na saa nane usiku wa kuamkia Jumatatu Septemba Mosi, 2025 kwa saa za Kenya.
Ajali hiyo katika barabara ya Kenscoff-Pétion-Ville eneo la Pèlerin 9 ilitokea wakati wa operesheni ya kuokoa gari iliyohusisha magari mawili ya kivita aina ya MaxxPro.
Ilisababisha kifo cha afisa huyo wa Kenya na raia wawili, huku maafisa wengine wanane wa MSS wakijeruhiwa. Watatu kati ya waliojeruhiwa wameripotiwa kuwa katika hali mahututi na wanapokea matibabu hospitalini.
Ndugu wa marehemu tayari wamearifiwa, na mipango ya kusafirisha mwili wake hadi Kenya inaendelea. NPS imetoa rambirambi zake za dhati kwa familia ya marehemu na kuahidi msaada kamili wakati huu mgumu.
MSS kwa kushirikiana na Polisi wa Kitaifa wa Haiti inaendelea kusimamia oparesheni hiyo inayolenga kurejesha amani na usalama nchini Haiti.
“Kama huduma, tumejikita katika kuhakikisha amani na usalama wa kudumu kwa watu wa Haiti” alisema Muchiri Nyaga Msemaji wa NPS akiongeza kwamba uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea.