Watu wanne wanaoshukiwa kuwa wezi waliovamia maghala ya Rama homes mapema jana walikamatwa na maafisa wa polisi kufuatia oparesheni ya maafisa wa kaunti ndogo ya Embakasi kwa ushirikiano na wananchi.
Polisi waliokuwa wakitumia habari walizopokea walikamata Patrick Mwangi Njue, Patrick Kariuki Karobia, Emmanuel Masika Bichi na Thomas Mucho Sikulova wakiendelea kupakia magunia ya dengu kwenye lori lenye nambari ya usajili KAS 148Q.
Matukio hayo yalinakiliwa huku ushahidi muhimu ukikusanywa na washukiwa kutiwa mbaroni wakisubiri kufikishwa mahakamani.
Wakati huo huo maafisa wa upelelezi wamekamatwa washukiwa wanne zaidi wa wizi wa mifugo katika maeneo ya kati na mashariki mwa Kenya.
Washukiwa watatu kati yao ambao ni John Macharia Karani, Martin Mwangi Gatimu na Charles Kariuki Njeru walikiri kuiba ng’ombe mmoja huko Kerugoya, wakamchinja na kusafirisha nyama hadi Embu ambapo iliuzwa.
Wapelelezi walipata gari aina ya Toyota Probox nambari KBT 117T, ambalo walitumia kusafirisha nyama hiyo.
Agustino Kiribi Mutea mmiliki wa duka la kuuza nyama la Capital alikamatwa mjini Embu baada ya kubainika kununua kilo 119 za nyama kutoka kwa washukiwa.