Serikali inakabiliwa na changamoto katika ukaguzi wa madeni yanayodaiwa iliyokuwa bima ya kitaifa ya afya NHIF.
Rais William Ruto amesema kwamba imekuwa vigumu kuhakiki madeni ya shilingi bilioni 30 ambayo NHIF inadaiwa baada ya kuvunjiliwa mbali.
Akizungumza jana huko Siaya, kiongozi wa nchi alielezea kwamba hospitali zimekuwa zikizuia juhudi za serikali za kwenda mahakamani kutafuta uhakiki wa madeni hayo.
Ruto alisema kwamba hakuna pesa zitalipwa hadi mpango wa uhakiki utekelezwe na kukamilishwa.
Rais alisema pia kwamba kuwekwa kwa shughuli za halmashauri ya afya ya jamii SHA katika mfumo dijitali kumewezesha utambuzi wa ulaghai haraka.
Kiongozi wa nchi aliambia wanaofuja raslimali za umma kwamba muda wao umekwisha na watakabiliwa kisheria watakapopatikana na watahitajika kurejesha pesa zote ambazo waliiba.
Rais alitaja hospitali elfu moja ambazo zimepokonywa leseni za kuhudumu kwa makosa ya kuilaghai SHA akisema wahusika watafikishwa mahakamani.
Kulingana naye kufuta leseni za taasisi hizo za afya kulikuwa hatua ya kwanza ya kuhakikisha uaminifu katika madai ya malipo kutoka SHA na itafuatiwa na hatua ya kuzidai pesa hizo kabla ya kushtaki wahusika.
Haya yanajiri wakati ambapo wabunge wanashinikiza waziri wa Afya Aden Duale ajiuzulu na kutishia kuanzisha mchakato wa kumbandua bungeni iwapo hatajiuzulu.
Ni wakati ambapo pia aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ametaja bima ya Afya ya SHA kuwa ulaghai.