Ruto: Wakenya wasioweza kumudu SHA kulipiwa na serikali

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto akiwa na Naibu Rais Kithure Kindiki katika Ikulu ya Nairobi walipokutana na viongozi kutoka Meru
Serikali itaanza kuwatolea Wakenya wasioweza kujimudu kifedha michango yao kwa Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA.
Rais William Ruto amesema mpango huo unafuatia mchakato uliofanikiwa wa kuwatambua watu wenye mahitaji.
Amesema hatua hii itahakikisha hakuna atakayeachwa nje ya mpango wa huduma za afya kwa wote, UHC.
Ameelezea kuwa wale walio na uwezo wa kulipa wanatoa mchango wa asilimia 2.75 wa mapato yao, na hivyo kuufanya mpango huo kuwa wenye usawa.
Rais amesema kwa misingi hiyo, serikali imekuwa ikikusanya fedha za kutosha kulipia wale wasiojiweza.
“Hazina ya Bima ya Afya ya Kitaifa (NHIF) ilikuwa na ubaguzi. Mama Mboga alikuwa analipa shilingi 500, sawa na asilimia 10 ya mapato yao. Nilikuwa nalipa shilingi 1,700, ambayo ilikuwa sawa na asilimia 0.01 ya mshahara wangu. Hii haikuwa sawa,” alisema Rais.
Ruto aliyasema hayo wakati wa mkutano na viongozi wa mashinani kutoka kaunti ya Meru waliomtembelea katika Ikulu ya Nairobi.
Naibu Rais Kithure Kindiki, Gavana wa Meru Isaac Mutuma, kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Kimani Ichung’wah, wabunge na wawakilishi wadi ni miongoni mwa waliokuwapo.
Rais Ruto alisema hadi kufikia sasa, SHA imeandikisha Wakenya milioni 25.8 ikilinganishwa na NHIF, ambayo ilikuwa na wanachama milioni 7 pekee.
Akielezea kuwa SHA inawahudumia Wakenya wote waliojiandikisha, kiongozi wa nchi amesema huduma zinazotolewa kwa wagonjwa wa kutwa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za kaunti ndogo ni za bure.
Share This Article