Naibu Rais Kithure Kindiki amesema Kenya imethibitisha tena kujitolea kwake kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika juhudi za maendeleo na mageuzi ya kiuchumi.
Alisema hayo wakati wa awamu ya 13 ya kikao cha ushirikiano wa kimaendeleo kilichofanyika katika makazi yake rasmi mtaani Karen.
Akihutubia mkutano huo wa ngazi ya juu, Kindiki alisisitiza juhudi zinazoendelea za Kenya kuimarisha ushirikiano unaolingana na vipaumbele vya kitaifa, hasa Ajenda ya Mageuzi ya Kiuchumi Kutoka Chini Kwenda Juu (BETA).
Alieleza kwamba kutengeneza fursa za ajira na kuwawezesha vijana kiuchumi ni kipaumbele cha juu kwa serikali ya Kenya Kwanza.
“Ili kufanikisha malengo ya maendeleo ya mageuzi, Serikali inafanya tathmini ya miradi inayoendelea kuhakikisha inachangia kwa ufanisi katika utoaji wa ajira na maendeleo ya uchumi,” alisema Kindiki.
Naibu Rais alieleza umuhimu wa utofauti wa kiuchumi kupitia kuunga mkono sekta ya kibinafsi, hasa katika viwanda, kilimo, na maeneo mengine muhimu ya maendeleo.
Aliongeza kuwa kuvutia uwekezaji wa ndani na wa kigeni ni muhimu katika kupanua wigo wa ushuru na kuunda ajira endelevu.
Kindiki alisifia kikao cha ushirikiano wa kimaendeleo akikitaja kuwa jukwaa muhimu la kutathmini athari za Msaada Rasmi wa Maendeleo (ODA) na jinsi unalingana na malengo ya kimkakati ya Kenya.
Alisisitiza tena dhamira ya serikali kuendeleza mageuzi ya kiuchumi na kiutawala, matumizi bora ya raslimali, na uwajibikaji.
Kikao hicho kiliwakutanisha wadau wakuu, wakiwemo washirika wa maendeleo, kujadili maendeleo ya Kenya katika utekelezaji wa misaada na mageuzi.
Naibu Rais alihitimisha kwa kusisitiza nia ya Serikali kuimarisha mifumo ya uwajibikaji na kuhakikisha matumizi bora ya msaada wa maendeleo.