Mahakama yaipa serikali siku 5 kuhusu Mpina kugombea urais Tanzania

Martin Mwanje
2 Min Read

Mahakama Kuu ya Tanzania imetoa muda wa siku tano kwa Serikali kujibu kesi iliyofunguliwa na chama cha ACT Wazalendo na Luhaga Joelson Mpina dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Uamuzi huo umetolewa leo, Agosti 28, 2025, na Mahakama kuu, Masijala kuu Dodoma, baada ya ACT Wazalendo kudai kulikuwa na ukiukwaji wa Katiba, sheria na kanuni za uchaguzi wakati wa mchakato wa uteuzi wa wagombea urais uliohitimishwa Agosti 27.

Luhaga Mpina ailienguliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kufuatia pingamizi lililotolewa na mwanachama wa chama hicho, Monalisa Ndala.

Sababu kuu iliyoelezwa na Monalisa ni kwamba Mpina alipata uanachama Agosti 5, 2025, nje ya muda wa kisheria wa kuchukua fomu za kugombea ndani ya chama, ambapo ilipaswa kuwa kabla ya Mei 25, 2025.

Serikali iliomba Mahakama kuongezewa muda wa siku 14 ili kuandaa majibu yake, lakini ombi hilo limekataliwa na Mahakama, ikisisitiza kwamba majibu hayo lazima yawasilishwe ndani ya siku tano pekee.

Hata hivyo, Mahakama imeeleza kuwa endapo itabainika kuwa Tume ya Uchaguzi ilikiuka katiba na sheria, haitasita kutoa amri ya kumpa Mpina fursa ya kurejesha fomu na kushiriki tena katika uchaguzi wa urais.

Kwa kuzingatia maslahi mapana ya taifa, Mahakama imeagiza shauri hilo kusikilizwa kwa njia ya mtandao kuanzia Septemba 3, 2025, saa tatu asubuhi.

Share This Article