Spice Diana aelezea sababu ya kukosa tamasha la Sheebah Karungi

Spice amesema kwamba siku ya tamasha hilo, alikuwa na onyesho jingine nje ya jiji la Kampala.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Sheebah Karungi aliandaa tamasha kubwa tarehe 22 mwezi huu wa Agosti mwaka 2025 ambalo alilipa jina la “The Return of the Queen”.

Tamasha hilo lilihudhuriwa na wasanii kadhaa wa Uganda waliotumbuiza lakini Spice Diana hakuwepo na sasa anaelezea sababu ya kutokuwepo.

Diana alisema kwamba ugomvi unaoaminika kuwa kati yake na Sheebah Karungi haukuwa sababu yake ya kutohudhuria akiongeza kwamba sababu iliyomfanya akose haina uhusiano na ugomvi huo.

Msanii huyo alielezea kwamba hakuwa mjini Kampala wakati huo.

“Nilikuwa na maonyesho nje ya Kampala lakini niliona onyesho lake na lilikuwa zuri kwake na kwa mashabiki wake. Watu wasingeenda kama hawakuwa na nia ya kufurahia.” Alisema Diana.

Aidha, alizungumzia kauli za Sheebah zilizotolewa wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kabla ya tamasha, ambapo Sheebah aliwatuhumu baadhi ya wasanii kwa kutumia vyombo vya habari kuharibia wenzao.

Spice alikubaliana kwa kiasi fulani na maoni hayo, akieleza kuwa juhudi kama hizo hazina maana.

“Kama mtu ameandikiwa kung’ara, atang’aa tu. Anaweza kuwa sahihi kuhusu alichosema kwa sababu tumeona yakitokea. Wakati mwingine ukitengana na meneja, wanaanza kukupiga vita, hata wasanii wenzako mkikosana wanaweza kukupiga vita. Lakini hata bila ugomvi, mtu mwingine anaweza tu kuamua kukupinga.” Alimalizia mwimbaji huyo.

Share This Article