Wito kwa wahisani kusaidia gharama ya matibabu Vietnam

Martin Mwanje
1 Min Read

Familia moja katika eneo la Kibarani, kaunti ya Kilifi inawaomba wahisani kujitokeza na kuwasaidia na shilingi zaidi ya milioni 10 kugharimia matibabu ya mpendwa wao aliyepata ajali nchini Vietnam mwezi Juni mwaka huu.

Kulingana na Rehema Ismail, mkewe mgonjwa huyo, Suleiman Chibohe aliyekuwa akifanya kazi ya ualimu nchini Vietnam alipata ajali ya barabarani baada ya pikipiki aliyokuwa akiendesha akitoka kazini kuhusika katika ajali mbaya iliyomfanya kujeruhiwa vibaya.

Akizungumza na wanahabari nyumbani kwao, Rehema ameeleza kuwa kufikia sasa, familia imetumia zaidi ya shilingi milioni moja kugharimia matibabu yake, fedha walizozipata kupitia michango ya familia na wahisani mbalimbali.

Hata hivyo, fedha hizo hazijaweza kuendeleza matibabu yake kikamilifu.

Familia hiyo sasa inapitia wakati mgumu na kupata msongo wa mawazo kutokana na ugumu wa kufadhili matibabu ya mpendwa wao ikizingatiwa kuwa yupo mbali na familia yake.

Haya yanajiri huku shirika la kutetea haki za kibinadamu la ICPS likiitaka serikali kuimarisha sheria zinazohusu Wakenya wanaofanya kazi ughaibuni.

Share This Article