Gavana wa Kericho Erick Mutai aliyebanduliwa Agosti 15 anatarajiwa kufika mbele ya Bunge la Seneti kuanzia leo Jumatano ili kujitetea juu ya mashtaka yanayomkabili yaliyosababisha wawakilishi wadi katika bunge la kaunti hiyo kumtema wiki mbili zilizopita.
Gavana Mutai na Bunge la Kaunti hiyo wametafuta huduma za mawakili mashuhuri kuwasaidia kuvuta kamba upande wao.
Hata hivyo, kufikia mwisho wa vikao vya kusikiliza madai dhidi yake, ni Maseneta watakaomua mustakabali wa Gavana Mutai.
Katika uamuzi wake wiki jana, Maseneta walipinga kubuniwa kwa kamati maalum ya kusikiliza mashtaka dhidi ya Gavana huyo.
Hiyo ina maana kwamba Gavana huyo, aliyewahi kubanduliwa madarakani awali, atalazimika kujitetea mbele ya kikao cha Maseneta wote.
Agosti 15, jumla ya Wawakilishi Wadi 33 walipiga kura kuunga mkono hoja ya kumtimua Gavana Mutai madarakani, huku 14 wakiipinga kupitia mfumo wa kielektroniki.
Punde tu baada ya Spika wa bunge la kaunti ya Kericho Patrick Mutai kutangaza matokeo hayo, mzozo uliibuka baina ya wawakilishi wadi hao, huku baadhi yao wakipinga matokeo hayo.
Wawakilishi wadi wanaomuunga mkono Gavana huyo, walipinga upigaji kura kutumia mfumo wa kielektroniki, wakisema kulikuwa na wizi wa kura ili kufanikisha njama yao.
Gavana huyo aliondolewa mamlakani kwa madai ya ukiukaji wa katiba, utumizi mbaya wa mamlaka na ukosefu wa maadili.
Anadaiwa kufanikisha ulipaji wa shilingi milioni 85 kwa wanakandarasi na wasambazaji bidhaa kinyume cha sheria.
Awali, Gavana huyo alikuwa ametetewa na wakili wake mkuu Katwa Kigen, aliyewasihi wawakilishi wadi hao kumuokoa kutokana na tuhuma dhidi yake.