Trump amfuta kazi Gavana wa Benki Kuu kwa madai ya ulaghai

Cook anadaiwa kutoa habari zisizo za kweli katika makubaliano ya mikopo ya ununuzi wa nyumba.

Marion Bosire
2 Min Read
Lisa Cook

Rais wa Marekani Donald Trump amemwachisha kazi Gavana wa Benki kuu ya Marekani Lisa Cook, kufuatia madai ambayo hayajathibitishwa ya ulaghai kwenye mchakato wa mikopo ya ununuzi wa nyumba.

Katika barua iliyochapishwa Jumatatu usiku, Trump alisema Cook, ambaye ni mmoja wa wanachama wa bodi ya benki hiyo anafutwa kazi mara moja kulingana na mamlaka ya Rais katika katiba ya Marekani na sheria ya benki kuu ya mwaka 1913.

Akitaja madai yaliyoibuliwa wiki iliyopita na mdhibiti wa mikopo ya ununuzi wa nyumba, Trump alisema kuna sababu tosha za kuamini kwamba Lisa alitoa taarifa za uwongo kwenye makubaliano ya mikopo hiyo ya ununuzi wa nyumba.

Trump alizungumzia jukumu la benki hiyo la kuweka viwango vya riba na hivyo raia wa Marekani wanafaa kuwa na imani na maafisa waliopatiwa jukumu la kutunga sera na kusimamia hazina ya kitaifa.

Trump alikuwa ametishia Ijumaa kwamba atamfuta Cook ambaye awali alikuwa mhadhiri wa chuo kikuu cha Michigan na ambaye aliteuliwa kwa wadhifa huo na Rais wa zamani Joe Biden, iwapo hatajiuzulu.

Iwapo Trump atafanikiwa kumwondoa afisini Gavana Cook, bodi ya benki kuu itasalia na fursa mbili kufuatia kujiuzulu kwa Gavana Adriana Kugle mwanzo wa mwezi huu.

Hatua hiyo itampa Trump kujaza bodi na wingi wa wateule wake.

Share This Article