Dogo Janja achunguzwa kwa kupiga mtu risasi

Msanii huyo anayewania udiwani anadaiwa kufanya hivyo kama njia ya kujikinga na hatari.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania Abdulazizi Abubakari Chende maarufu kama Dogo Janja, anaendelea kuchunguzwa na maafisa wa polisi nchini Tanzania kufuatia kisa ambapo anadaiwa kumpiga risasi mtu mmoja huko Arusha.

Katika taarifa kamanda wa polisi katika mkoa wa Arusha alisema, “Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linafanya uchunguzi kuhusiana na tukio la mtu mmoja aitwaye Bakari Halifa Daud (18) mkazi wa Sombetini Jijini Arusha kujeruhiwa kwa kupigwa risasi mguuni.”

Kulingana na kamanda huyo, uchunguzi wa awali umebaini kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 23, 2025 saa tano unusu usiku katika maeneo ya Sombetini Jijini Arusha.

Dogo ambaye anawania Udiwani anaripotiwa kufyatua risasi hiyo kama njia ya kujikinga na hatari wakati Bakari na mwenzake walimkabili wakati alikuwa nashuka kwenye gari lake.

“Wakati Abdulazizi Abubakari (30) mkazi wa Levolosi Jijini Arusha akiwa anashuka kwenye gari kudai kutaka kuvamiwa na Bakari Halifa akiwa na mwenzake kwa kutumia silaha ya jadi” iliendelea kusema taarifa ya kamanda.

Kamanda wa polisi anasema uchunguzi unaonyesha Dogo Janja alilazimika kutumia silaha aliyokuwa nayo kujiepushia hatari.

“Aidha watu wawili wanashikiliwa kuhusiana na tukio hili, uchunguzi unaendelea.” Alimalizia Kamanda huyo wa polisi katika mkoa wa Arusha.

Share This Article