Mbosso azuru mwalimu aliyebadili wimbo wake

Mwalimu huyo aliimba wimbo PAWA upya ambapo alibadili maneno yake kidogo na kuyafanya kuwa ya kuwatia wanafunzi moyo wa kusoma kwa bidii.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania Mbwana Yusuf Kilungi maarufu kama Mbosso alifunga safari kutoka Dar es Salaam hadi kijijini Kazita kumzuru mwalimu aliyebadili wimbo wake wa PAWA na kuufanya kuwa wa kuwatia wanafunzi hamasa.

Mbosso alinakili video za safari yake na watu wa kundi lake wakielekea kumtafuta mwalimu aitwaye Jao Mabruck Kalesi akazichapisha kwenye Istagram na kuandika “Takribani Kilometa 298 na zaidi kutoka Dar Es Salaam hadi kufika Wilaya ya Muheza ( Muheza Mjini ) hazikutosha kumfikia Mwalimu Wetu wa #PAWA”.

Aliendelea kusimulia jinsi walilazimika kusafiri kilomita nyingine zaidi ya 40 kabla ya kufika eneo la milimani Katika Kijiji Cha KAZITA walikopatana na Kalesi na wanafunzi wake.

“Lengo ni kuthamini na kuwafikiashia Pongezi na Zawadi kama Mrejesho wa Shukrani kwa Kuufanya Wimbo Wetu Wa #PAWA kuwa Sehemu ya Hamasa ya kufundishia wanafunzi na kuwatia Moyo Kwenye Masomo Yao” aliandika Mbosso.

Aina ya mwalimu Kalesi ya wimbo huo wa PAWA sasa inatumiwa na walimu wengine nchini Tanzania kama njia ya kuwatia moyo waweze kufanya vyema kwenye masomo yao.

Mbosso alimpongeza Mwalimu Kalesi na wanafunzi wa shule ya msingi ya Kazita kwa kile alichokitaja kuwa ubunifu huku akiwaombea barka kwa Mungu.

Share This Article