Vita dhidi ya ufisadi vinaonekana kupamba moto nchini huku tume ya maadili na kupambana na ufisadi EACC ikitangaza kwamba inachunguza maafisa kadhaa wakuu serikalini na kutwaa mali ya umma.
Katika taarifa kwenye mkutano na wanahabari leo, Afisa mkuu mtendaji wa EACC Abdi Mohamud alifichua kwamba tume hiyo imekamilisha uchunguzi wa kesi 89 za hadhi ya juu za ufisadi katika muda wa miezi minane iliyopita.
Tume hiyo imependekeza kushtakiwa kwa wahusika wa kesi 82 kati ya hizo.
Wahusika wa kesi hizo wanajumuisha magavana walio madarakani sasa, waliostaafu, mawaziri wawili wa zamani, katibu wa wizara na wasimamizi wa mashirika mbali mbali ya serikali.
Uchunguzi dhidi yao ulilenga matumizi mabaya ya fedha, kujipatia pesa kwa njia ya ulaghai, mkinzano wa maslahi pamoja na kuwa na mali ambayo asili yake haielezeki.
Tume hiyo ya kukabiliana naufisadi kwa sasa inachunguza magavana watano wanaohudumu sasa na 11 wa awali. Inachunguza pia wafanyakazi wa serikali za kaunti wapatao 822 katika sakata ya shilingi bilioni 1.6.
Sakata hiyo inahusisha malipo yaliyofanywa kwa njia isiyofaa na matumizi mabaya ya mikopo.
Kuanzia Januari, EACC imefanikiwa kurejesha mali ya serikali ya thamani ya shilingi milioni 600 na pesa taslimu shilingi milioni 105 huku ikizuia kupotea kwa bilioni 7.2.
Mohamud alitambua ghadhabu ya umma hasa miongoni mwa vijana kuhusu ufisadi uliokithiri lakini ameapa kuimarisha juhudi za kurejesha mali iliyoibwa na kuzuia wizi zaidi.