Serikali imeimarisha juhudi za kukabiliana na visa vya watu kujitoa uhai katika kaunti ya Nyeri na eneo zima la Mlima Kenya, vinayoaminika kusababishwa na matumizi ya pombe na mihadarati.
Akizungumza huko Nyeri katika kikao cha Jukwaa la Usalama, Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen alitaja maovu mengine yanayotokana na uraibu huo kama ubakaji na dhuluma za kijinsia.
Murkomen alisema serikali inabuni jopo la kitaifa litakalojumuisha maafisa wa mashirika kama mamlaka ya kukabiliana na pombe na mihadarati, NACADA, shirika la kukusanya ushuru nchini, KRA na lile la kukadiria ubora wa bidhaa, KEBS.
Jopo hilo litatwikwa jukumu la kupiga jeki juhudi za makundi ya usalama ya kaunti za kukabiliana na matumizi ya pombe na mihadarati.
Waziri Murkomen alisema kwamba kaunti ya Nyeri huwa tulivu na huwa inanakili visa vichache vya utovu wa usalama na juhudi za kukabiliana na pombe haramu zimefanikiwa pakubwa humo.
Hata hivyo, aliongeza kwamba kuna wafanyabiashara walaghai ambao wanauza pombe haramu, kemikali ya ethanol na bangi, vitu ambayo mtu akitumia kwa muda mrefu vinamsababishia matatizo ya kiafya.
Kikao cha Nyeri cha Jukwaa la Usalama kilikuwa cha 32.